USHETU YAAZIMIA KUTOKOMEZA DARAJA SIFURI KWA KIDATO CHA NNE IFIKAPO 2025 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 8 May 2025

USHETU YAAZIMIA KUTOKOMEZA DARAJA SIFURI KWA KIDATO CHA NNE IFIKAPO 2025

 

Mwenyekiti wa baraza la madiwani Gagi Lala akizungumza katika baraza hilo ambapo amewasisitiza madiwani kwenda kusimamia miradi iliyobaki na kuhakikisha inakamilika


NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL USHETU


Halmashauri ya Ushetu, iliyopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imeazimia kwa dhati kutokomeza kabisa daraja sifuri kwa wanafunzi wa kidato cha nne kuanzia mwaka huu wa 2025, Hatua hii ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda na kuleta mabadiliko chanya kwa jamii ya Ushetu. 


Azimio hilo limebainishwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Mei 7, 2025, ambapo viongozi mbalimbali wa halmashauri hiyo walieleza mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya elimu.


Diwani wa Kata ya Kinamapula, Sharifu Samwel, ameeleza kuwa moja ya mbinu wanazotumia ni kuboresha miundombinu ya madarasa katika shule za sekondari pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa walimu wa kutosha. 


Samwel amesema uwepo wa walimu wengi unasaidia kupunguza mzigo wa kazi kwa walimu mmoja mmoja na hivyo kuongeza ufanisi katika ufundishaji, jambo linalosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja sifuri.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyankende, Doa Limbu, ameeleza kuwa Halmashauri ya Ushetu iliwahi kushika nafasi ya mwisho miongoni mwa halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga, Hata hivyo, jitihada walizozifanya zimezaa matunda kwani kwa mwaka huu wamefanikiwa kushika nafasi ya kwanza.

Limbu amesema kuwa changamoto kama utoro, kuchelewa kuanza masomo kwa baadhi ya watoto katika muhula wa masomo, pamoja na upungufu wa madarasa, zimekuwa zikirudisha nyuma maendeleo ya elimu, lakini sasa wanazitatua hatua kwa hatua.


Naye Diwani wa Viti Maalum, Esta Matone, ametumia kikao hicho kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu ya madarasa, Pia amesema kuwa wazazi sasa wamehamasika zaidi na wanahakikisha watoto wao wanahudhuria shule kikamilifu.


Matone amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mzazi kuendelea kuwaunga mkono watoto ili waepukane na ujinga na kuhakikisha ufaulu wa juu unapatikana.


Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani, ameeleza kuwa awali halmashauri hiyo ilikuwa na zaidi ya wanafunzi 200 waliopata daraja sifuri, lakini kutokana na mikakati madhubuti, idadi hiyo imepungua hadi kufikia 43 pekee.

 
Cherehani amebainisha kuwa mkakati wao mkubwa ni kutokomeza kabisa daraja la mwisho, na tayari kuna mafanikio makubwa ambapo zaidi ya wanafunzi 104 wamepata daraja la kwanza, baadhi yao wakiwa na pointi 7.


Mbunge Cherehani pia ameeleza kuwa shule mpya tano za sekondari zimejengwa katika halmashauri hiyo, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza fursa za elimu bora kwa vijana wa Ushetu, Shule hizi mpya ni kielelezo cha dhamira ya serikali kuwekeza katika elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi sawa ya kufaulu.


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ameweka mkazo katika umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kwani mtoto wa kike anapaswa kupata elimu na kufaulu ili awe na thamani katika jamii. 

Mhita ameonya dhidi ya ndoa za utotoni na kuwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mabinti wanamaliza masomo yao huku akisisitiza kuwa elimu ndiyo njia ya kumkomboa mtoto wa kike.


Mhita amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu kufuatilia shule zenye maeneo makubwa ya mashamba ili kuweka mkakati wa kuzalisha chakula cha wanafunzi Lengo ikiwa ni kuhakikisha watoto wanapata lishe bora shuleni, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wao wa kujifunza na kufaulu.


Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akiwasisi madiwani kuwahamasisha wazazi kuhakikisha  watoto wanamaziza masomo wakiwa na ufaulu mzuri
Mwenyekiti wa baraza la madiwani Gagi Lala akizungumza katika baraza
Mwenyekiti wa baraza la madiwani Gagi Lala akizungumza katika baraza hilo ambapo amewasisitiza madiwani kwenda kusimamia miradi iliyobaki na kuhakikisha inakamilika
Mkurugenzi wa halmashauri ya Ushetu ambaye ni katibu wa baraza la madiwani wa jimbo hilo, Bi Hadija Kabojela akizungumza katika kikao cha baraza hilo.

Madiwani wa jimbo la Ushetu wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso