Na: Paul Kasembo – Mwakitolyo, Shinyanga DC
Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Anamringi Macha, imethibitisha kutokea kwa ajali katika mgodi wa dhahabu uliopo Kitalu Namba 8, Kijiji cha Nyaligongo Namba 2, Kata ya Mwakitolyo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambapo watu sita (6) wamepoteza maisha na wengine kumi na moja (11) kujeruhiwa.
RC. Macha alitoa taarifa hiyo Mei 18, 2025 alipowasili eneo la tukio na kuwapa pole wahanga wa ajali hiyo pamoja na familia zao, huku akisisitiza kuwa Serikali inatambua, inathamini na inaheshimu sana shughuli zinazofanywa na wachimbaji wadogo, na itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha usalama wao unalindwa wakati wote.
"Tumekuja kuwapa pole kwa niaba ya Serikali. Ninathibitisha kuwa jumla ya watu sita wamefariki dunia na wengine kumi na moja kujeruhiwa. Mmoja kati ya majeruhi hao ameshatibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani, huku wengine kumi wakiendelea kupokea matibabu hospitalini. Serikali itaendelea kutoa huduma stahiki kwa wahanga wa tukio hili," alisema RC. Macha.
Kwa ujumla, ajali hiyo ilitokea mnamo Mei 17, 2025 kuanzia majira ya saa 5:00 asubuhi, ambapo juhudi za uokoaji zilianza mara moja. Serikali inasisitiza kuwa idadi rasmi ya vifo na majeruhi ni kama ilivyotangazwa na si vinginevyo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, sambamba na kuweka mikakati ya kuimarisha usalama na kuboresha mazingira katika shughuli za uchimbaji madini hususan kwa wachimbaji wadogo wote mkoani Shinyanga wakiwemo hao wa Mwakitolyo.
No comments:
Post a Comment