Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akitazama maendeleo ya zoezi la udhibiti wa magugumaji ndani ya Ziwa Victoria eneo la Kigongo Feri wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Mei 19, 2025. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mha. Cyprian Luhemeja alipokuwa akikagua shughuli za udhibiti wa magugumaji Ziwa Victoria katika eneo la Kigongo Feri wilayani Misungwi hadi Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Mei 19, 2025.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya zoezi la udhibiti wa magugumaji ndani ya Ziwa Victoria eneo la Kigongo Feri wilayani Misungwi hadi Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Mei 19, 2025.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi alipokuwa akikagua shughuli za udhibiti wa magugumaji Ziwa Victoria katika eneo la Kigongo Feri wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Mei 19, 2025.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya zoezi la udhibiti wa magugumaji ndani ya Ziwa Victoria eneo la Kigongo Feri wilayani Misungwi hadi Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Mei 19, 2025. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa Magugumaji katika Ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii kuendelea katika maeneo hayo.
Ameyasema hayo Mei 19, 2025 wakati akizungumza na wananchi alipokuwa akikagua shughuli za udhibiti wa magugumaji katika eneo la Kigongo Feri wilayani Misungwi mkoani Mwanza ambapo amesema hali ya uwepo wa gugumaji kama ingeachwa ingepunguza ukubwa wa ziwa na kusababisha kupunguza shughuli za binadamu.
“Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha zaq ununuzi wa mitambo mikubwa ya shuguli za uvuvi, usafi na usafirishaji kuendelea.”
“Vivuko vyetu vilikuwa vikipita vinakula gugumaji na kusababisha tatizo lingine na hali hiyo kama ingeachwa na kuongezeka ingefunika ziwa na kusingekuwa na shughuli za uvuvi ambayo inategemewa na wengi.
“Hali hii ilipojitokeza tuliagiza zichukuliwe hatua ya haraka za kupambana na magugu lakini pili kuwa na mpango wa muda mfupi, mpango wa kati na mpango wa muda mrefu ili kunusuru ziwa letu na kuruhusu shughuli ziendelee,” amesema Mhe. Majaliwa.
Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi, Cyprian Luhemeja amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa maelekezo na miongozo katika kushughulikia changamoto ya gugumaji.
Amesema katika utekelezaji wa mkakati wa uondoji magugumaji mchakato wa manunuzi wa mitambo miwili maalum ya kuopoa gugumaji aina ya Salvinia na mtambo mkubwa wa kuondoa gugumaji aina ya Lutenda umekamilika na mitambo hiyo inatarajia kufika mwishoni mwa mwezi Julai, 2025.
Mha. Luhemeja amesema katika kushughulikia changamoto hiyo kwa kipindi cha muda mfupi Jumla ya tani 840 za gugumaji jipya aina ya Salvinia molesta limeopolewa na kufungua njia ya usafiri na shughuli za kiuchumi katika eneo la Kigongo-Busisi. Kwa sasa eneo hili halina changamoto tena ya Gugumaji ya aina hii mpya.
“Juhudi zinaendelea katika eneo hili la Kigongo-Busisi za kushughulikia gugumaji la asili aina ya Lutende. Jumla ya Ekari 65 zimeshughulikiwa katika kipindi cha wiki moja na lengo ni kumaliza Ekari zote kabla ya tarehe 10 ya Mwezi Juni-2025.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Menan Jangu akisoma taarifa ya Kamati ya Kuondoa Magugumaji Ziwa Victoria amesema gugumaji limegawanyika katika aina tatu ambalo ni gugumaji jipya aina ya salivinia molesta, Water Hyacinth na gugumaji la asili aina ya Lutende.
Ameongeza kuwa magugumaji haya yameathiri mifumo ya ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria. Katika hatua za muda mfupi zoezi la uopoaji lilianzia katika eneo la Kigongo-Busisi kwa kuopoa gugumaji aina ya Salvinia molesta kwa kutumia mitumbwi na matenga.
“Kwa kipindi cha Mwezi Februari hadi kufikia tarehe 18 Mei 2025 kiasi cha tani 840 kimeopolewa na zoezi hili limesaidia kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika eneo la Kigongo-Busisi na tayari gugumaji aina ya Water Hyacinth limekwishadhibitiwa na Serikali kwa juhudi zilizofanywa kupitia Bonde la maji la Ziwa Victoria.
“Kwa sasa Eneo letu la ziwa linakabiliwa na Gugu maji la asili aina ya Lutende. Pamoja na faida za mimea ya asili ya Lutende katika hifadhi ya bioanuai na kuchuja maji yaingiayo ziwani, mimea hii inapokatika na kuacha eneo lake la asili na kuingia ziwani inaathiri shughuli za usafiri na usafirishaji pamoja shughuli za uvuvi kwa wananchi” amesema Dkt. Jangu.
Dkt. Jangu amesema eneo la Kigongo-Busisi kiasi cha Ekari 375 la ziwa limeathirika na Gugu hili aina ya Lutende, gugu ambalo linaonekana katika maeneo mengi ya Ziwa Victoria na hivyo limeathiri kwa sehemu kubwa shughuli za uchumi kwa wananchi katika maeneo husika.
No comments:
Post a Comment