Na Berenc China, Bariadi
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kimefanya mkutano mkuu maalum wa kutathmini na kutangaza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020, hususan kazi zilizofanywa na Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Mheshimiwa Kundo Andrea, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama wa chama hicho, viongozi wa serikali, na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi, alimtaja Mheshimiwa Kundo Andrea kuwa ni miongoni mwa wabunge wachapakazi walioweza kuleta maendeleo ya dhahiri katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ndani ya jimbo hilo.
"Ninatoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Mbunge Kundo Andrea kwa kazi kubwa na yenye matokeo makubwa kwa wananchi wa Bariadi. Serikali inatambua juhudi zake hasa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwemo sekta za elimu, afya, maji na barabara," alisema Kihongosi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bariadi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Kundo Andrea, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani akibainisha mafanikio yaliyopatikana kutokana na usimamizi wake wa karibu katika miradi ya maendeleo.
"Tumefanikisha ujenzi na upanuzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya jimbo hili, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto ya watoto kusafiri umbali mrefu kufuata elimu. Vilevile, tumepanua huduma za afya kwa kujenga na kukarabati vituo vya afya, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama," alisema Andrea.
Aliongeza kuwa juhudi hizo zinalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo hawakusita kutoa pongezi kwa Mbunge wao, wakieleza kuwa wameona mabadiliko chanya tangu alipochaguliwa kuliongoza jimbo hilo. Pia walieleza matumaini yao ya kuendelea kuona kasi hiyo ya maendeleo ikiendelea katika miaka ijayo.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa maazimio ya kuendelea kushirikiana kwa karibu kati ya wananchi, chama, na serikali katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi yote inayolenga kuinua ustawi wa jamii ya Bariadi unaendelea kwa ufanisi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment