WANACHAMA ZAIDI YA LAKI MOJA WA CCM KAHAMA KUPATA KADI ZA KIELEKTRONIKI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 25 April 2025

WANACHAMA ZAIDI YA LAKI MOJA WA CCM KAHAMA KUPATA KADI ZA KIELEKTRONIKI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 



NA NEEMA NKUMBI - KAHAMA


Zaidi ya wanachama hai 101,000 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama wanatarajia kupokea kadi za uanachama za kielektroniki katika zoezi maalum lililopewa jina la Siku Kumi za Moto, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wa madiwani, wabunge, na Rais.


Akizungumza leo na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Ndugu Andrew Chatwanga, amesema kuwa zoezi hilo limeanza rasmi leo na linatekelezwa kwa muda wa siku kumi, likilenga kuwafikia wanachama laki moja kwa awamu ya sasa. Aidha, amebainisha kuwa katika awamu zinazofuata, CCM inalenga kuwafikia wanachama wengine takribani laki nne, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wanachama wote wanakuwa na kadi za kisasa.


“Tunataka kuona kila mwanachama anakuwa na kadi ya kielektroniki ambayo itampa uhalali wa kushiriki shughuli zote za chama, ikiwa ni pamoja na upigaji kura wa ndani ya chama,” amesema Chatwanga.


Baadhi ya wanachama waliopokea kadi hizo wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema kuwa kadi hizo zitawarahisishia utambulisho na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za kichama.


Katika kuwahamasisha wanachama, Chatwanga ametoa wito kwa wote kufika katika vituo vilivyopo kwenye matawi yao ili kuchukua kadi hizo. 

Chatwanga ameongeza kuwa Wilaya ya Kahama ina wanachama wapatao laki sita waliotapakaa kwenye jumla ya matawi 323, hivyo ni muhimu kila mwanachama kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.


Chatwanga amesema CCM itahakikisha maandalizi ya uchaguzi mkuu yanafanyika kwa uwazi na kwa kuimarisha misingi ya ushirikishwaji wa wanachama wake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso