
Mfanyabiashara wa Vyuma Chakavu Akamatwa na Mita za Maji Kahama – KUWASA Yapata Hasara ya Milioni 25
NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Rajabu Msimbe, mkazi wa Mtaa wa Majengo na mfanyabiashara wa vyuma chakavu, kwa tuhuma za kupatikana na mita mbili za maji mali ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA), zilizokuwa zimefichwa ndani ya mzigo wa vyuma chakavu.
Tukio hilo limebainika katika Mtaa wa Mhongolo kufuatia taarifa za siri kutoka kwa wasamaria wema, zilizopelekea kufanyika kwa upekuzi wa kushitukiza ulioshirikisha jeshi la polisi na maafisa wa KUWASA.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Uhusiano wa KUWASA, John Mkama, amesema kuanzia mwezi Oktoba 2024 hadi Aprili 23, 2025, jumla ya mita 210 za maji zimeibiwa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kahama, na kusababisha hasara ya Shilingi milioni 25.2.
“Dira hizi zina thamani ya shilingi 120,000 kila moja, na kuibiwa kwa kiasi hiki ni pigo kubwa kwa mamlaka na wananchi wanaotegemea huduma ya maji,” amesema Mkama.
Mkama ameongeza kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kutasaidia kufichua mtandao unaohusika na wizi huo, ikiwemo kujua soko la vifaa hivyo na waliko wateja wake.
“Huyu tuliyemkamata anaweza kufichua wapi mita hizi hupelekwa, nani anayezihitaji na matumizi yake, Hii ni hatua kubwa ya kuelekea kuvunja mtandao huu,” ameeleza Mkama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mhongolo, Charles Nangale, amelaani vikali tukio hilo na kutoa wito kwa wanunuzi wa vyuma chakavu kuacha kabisa kununua nyara za serikali.
“Ni kosa kubwa kununua vifaa vya serikali. Hii miundo mbinu ya maji ni muhimu kwa wananchi, Msako upo na tutawakamata wote wanaohusika,” amesema Nangale.
Hata hivyo, Rajabu Msimbe alikana kuhusika moja kwa moja na ununuzi wa dira hizo, akisema zilinunuliwa na kijana wake bila yeye kuwepo, na zilikuwa zimehifadhiwa kwenye mfuko zikiwa hazijawekwa wazi.
“Sikuwepo wakati wa ununuzi, na hatuna utaratibu wa kununua dira za maji, Zilikutwa zimechanganywa na vyuma vingine,” amedai Msimbe.
Baadhi ya wakazi wa Kahama, akiwemo Shakira Mohamedi na Sharifu Katala, walitoa rai kwa serikali kuchukua hatua kali kwa wote wanaohusika na wizi huo, wakisema kuwa uharibifu wa vifaa vya huduma za msingi unaathiri jamii kwa ujumla.
“Tuchukue hatua, Wakamatwe, watajane, ili iwe fundisho kwa wengine maana Mamlaka zinapata hasara na sisi wananchi tunakosa huduma,” wamesema wakazi hao.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini genge zima linalojihusisha na wizi na biashara ya nyara za serikali ikiwemo mita za maji, nyaya na vifaa vingine vya taasisi za umma.




No comments:
Post a Comment