Rais wa Zanzibar Na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali kuendelea na juhudi za kuleta Maendeleo wananchi katika kila sekta  na kuwaomba kuunga mkono katika juhudi hizo.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 1 Oktoba 2024  wakati  alipojumuika na Waumini wa  Dini ya Kiislamu  katika Maulid ya Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) , Tumbatu Jongowe Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais Dk Mwinyi  amefahamisha kuwa lengo la Serikali ni  kuona  Wanafunzi nchi mzima wanasoma  katika mazingira rafiki  ,majengo ya kisasa yenye  vifaa kamili vya kufundishia , maabara,  vyumba vya Kompyuta .
Aidha  Rais Dk.Mwinyi  amebainisha kuwa Serikali inakusudia kujenga hospitali ya Wilaya ili wananchi wa  Tumbatu kuwa na Uhakika wa matibabu na kuwapunguzia gharama za kufuata matibabu katika maeneo mengine.
Akizungumzia suala la malezi ya  vijana na Watoto ametoa wito kwa Wazazi kuweka mkazo katika kuwafundisha maadili na malezi bora ili wawe raia wema wa baadae .
Amesisitiza kuwa Amani ndio msingi wa Maendeleo ya  nchi inayohitaji kuleta Maendeleo hivyo kila mmoja ana jukumu la kulinda Amani.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amewahakikishia wananchi wa Tumbatu  kuwa Serikali  itajenga  skuli nyengine kubwa kisiwani  humo ili kukidhi mahitaji  na kuwawezesha Wanafunzi kusoma katika mazingira Bora.
Wakati huo huo  Rais  Dk. Mwinyi amekabidhi shillingi Milioni nane kwa Zawiyya nne za Tumbatu kwa ajili ya maandalizi ya Maulidi ya Mtume .

No comments:
Post a Comment