MCHELE KUTOKA MAREKANI NI SALAMA-TBS - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday 18 March 2024

MCHELE KUTOKA MAREKANI NI SALAMA-TBS

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema msaada wa chakula ulitolewa na Wizara ya Kilimo ya Marekani umefuata taratibu za kuingizwa nchini na ni salama kwa matumizi ya binadamu.



Taarifa hiyo ya TBS ilitolewa jana Machi 17, 2024 kufuatia sintofahamu iliyotokana na chakula hicho kuongezwa virutubisho kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji.


“Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuihusiana na msaada wa chakula (mchele ulioongezwa virutubisho, mafuta ya kupikia ya alizeti yaliyoongezwa virutubisho na maharage), ambao ulitolewa na Wizara ya Kilimo ya Marekani kwa ushirikiano na Taasisi ya Jumuiya ya Kimataifa (Global Communities) katika baadhi ya shule za mkoa wa Dodoma, chini ya mpango uitwao ‘Pamoja Tuwalishe’.


“TBS inapenda kuujulisha umma kuwa chakula hicho kilifuata taratibu za uingizwaji wa chakula nchini ambapo kilipofika kilifanyiwa ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa matumizi.


“Aidha, utaratibu wa kuongeza virutubishi kwenye chakula (food fortification) unakubalika kitaalamu na hufanyika kwa lengo la kuboresha hali ya lishe kwa walaji,” imesema taarifa ya TBS.

Tamko hilo la TBS, limekuja siku moja baada ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kusema kuwa wamewaambia Wamarekani kuwa aina ya msaada walioutoa unapatikana nchini.


Akizungumzia wakati wa kuelezea miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya kilimo, Waziri Bashe alisema juni Machi 17 kuwa Tanzania inazalisha mchele na maharage kwa kiwango cha kutosha, hivyo zile fedha wanazotumia kuwapa wakulima wa Marekani wawape Watanzania na virutubisho viwekwe hapa nchini.


“Zile fedha wanazotumia kuwapa wakulima wa Marekani wawape Watanzania, tununue mchele kutoka Tanzania, maharage kutoka hapa Tanzania, halafu hivyo virutubisho mnavyotaka kuweka muwekewe hapahapa Tanzania wote tunaona," alisema Bashe.


Waziri huyo aliongeza kuwa ameieleza NGO (taasisi isiyo ys kiserikali iliyotoa msaada huo) kuwa Tanzania inajitosheleza kwa chakula.


CREDIT: MWANANCHIDIGITAL

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso