TADEPA YASISITIZA UMUHIMU WA ELIMU KWA JAMII KATIKA KUKABILIANA NA UTAPIAMLO NA UDUMAVU KWA WATOTO WACHANGA UMRI MIAKA 0 HADI 8 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday 13 February 2024

TADEPA YASISITIZA UMUHIMU WA ELIMU KWA JAMII KATIKA KUKABILIANA NA UTAPIAMLO NA UDUMAVU KWA WATOTO WACHANGA UMRI MIAKA 0 HADI 8

Shirika lisilo la Kiserikali liitwalo TADEPA la mkoani Kagera limewahimiza halmashauri ya wilaya ya Missenyi, linapoweka mikakati mbalimbali katika kushughulikia afya ya watoto wadogo likiwapo suala la lishe katika kupambana utapiamlo na udumavu wawangalie watoto kuanzia miaka 0 hadi nane.



Na Mutayoba Arbogast, HUHESO DIGITAL, Bukoba


Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri y Missenyi, Tapita Tuvana Solomoni, Kushoto akiongoza Kikao cha Kamati ya Lishe.Kulia ni Mganga mkuu wa wilaya, Dk Daniel Chochole


Mratibu wa mradi wa Mtoto Kwanza katika shirika hilo la TADEPA (Tanzania Development and AIDS Prevention), Abimeleck Richard, ameyasema hayo hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya Lishe kwa robo ya pili mwaka 2023/24 kilichofanyika ukumbi mdogo wa halmashauri hiyo, kupokea na kujadili taarifa mbalimbali zinazohusu lishe.


Amesema wazazi na walezi wanahitaji sana kuelimishwa kuwa lishe bora na toshelezi inasaidia katika utengenezaji na ukuaji wa ubongo wa mtoto kuanzia miaka 0 hadi nane, katika kumtengeneza binadamu aliyekamilika.


Amesema tatizo kubwa siyo upungufu wa chakula katika kaya kwani mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi, bali elimu juu ya unyonyeshaji na kumlikiza mtoto, pamoja na uandaaji wa chakula, ni mambo ya msingi kuhusu lishe.


Halmashauri hiyo imeweka mikakati katika kukabiliana na lishe duni inayosababisha utapiamlo na udumavu.


Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Tapita Tuvana Solomoni, amesema wataendelea kutilia mkazo suala la elimu ya lishe katika jamii hasa kupitia Maadhimisho ya Siku ya Afya katika vijiji, ambapo mwaka 2023, maadhimisho hayo yalifanyika katika vijiji 74 kati ya 77, kuhimiza bustani za mbogamboga shuleni, utoaji wa Vitamin A kwa watoto chini ya miaka mitano nk


Respicius John, mkazi wa kata Nsunga ameyataka Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA) ambao pia ndio wanasimamia miradi ya maji wilayani Missenyi kuangalia fena usahihi wa bill zao za maji kwani hazilingani na uhalisia wa maji yaliyotumika, na hivyo kusababisha baadhi ya watu kutoyatumia maji ambavyo ingestahili, na hivyo kuathiri mchakato mzima wa utayarishaji chakula chenye lishe kwa ajili ya watoto.


Imamu wa msikiti wa BAKWATA Bunazi, Abullahimidu Abdallah,amesema upo umuhimu mkubwa wa kuletewa mashine za LUKU za kulipia kadri mtu alivyotumia maji, itaondoa manung'uniko ya matumizi ya maji, maana baadhi ya watumiaji maji wanapoambiwa ndoo moja ya plastiki ina lita 20, wao hujaza maji pomoni kwamba ndio lita 20,ila kiukweli kuna mahali kuna alama ya mkanda ambapo hapo ndio ujazo wa lita 20.



Afisa Lishe wa halmashauri hiyo, Faustina Godwin, amesema kuwa ataendelea kushirikiana na Kamati hiyo ya lishe kuhakikisha masuala ya lishe yanawafikia wananchi wote ikiwemo mikutano ya hadhara ya vitongoji na vijiji na shuleni pia.


Taarifa ya wilaya hiyo inaonesha kwa mwaka 2023 kulikuwa na watoto wenye umri chini ya miaka mitano 47,714 na kuwa mwaka huo huo asilimia 5 ya watoto waliozaliwa walikuwa na uzito pungufu yaani chini ya kilogramu 2.5



Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Lishe wakishiriki mjadala wa mikakati ya kuinua kiwango cha lishe

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso