BEI ZA PETROLI,DIZELI NA MAFUTA YA TAA ZAENDELEA KUSHUKA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday 7 February 2024

BEI ZA PETROLI,DIZELI NA MAFUTA YA TAA ZAENDELEA KUSHUKA

Watumiaji wa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa wanaendelea kupata ahueni na kupunguza kiwango cha fedha wanachotumia katika kununua bidhaa hiyo baada ya bei kuendelea kushuka nchini.


Kushuka kwa bei kwa mwezi Februari 2024 kunatajwa kuchangiwa na kupungua kwa bei katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia 10.66 kwa petroli, asilimia 11.20 kwa dizeli na asilimia 5.82 kwa mafuta ya taa.

Pia kupungua kwa bei za mafuta kumetokana na kushuka kwa gharama za uagizaji wa mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 9.69 kwa dizeli na asilimia 1.82 kwa mafuta ya taa.

Taarifa ya bei za kikomo inayoanza kutumika leo Februari 7, 2024 iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), inaeleza kuwa gharama za uagizaji wa mafuta ya petroli na dizeli kwa Bandari za Tanga na Mtwara, nazo zimepungua kwa wastani wa asilimia 0.69 na asilimia 11.93, mtawaliwa.

Kufuatia suala hilo, sasa wakazi wa jiji la Dar es Salaam watanunua lita moja ya mafuta ya petroli kwa bei isiyozidi Sh3,051 ikiwa ni pungufu kutoka Sh 3,084 iliyokuwapo awali.

Kwa upande wa dizeli, wakazi wa Dar es Salaam sasa watanunua lita moja bei isiyozidi Sh3,029 kutoka Sh3,078 za awali.

Kwa upande wa mafuta ya taa ambayo mwezi uliopita bei yake iliongezeka hadi kufikia Sh3, 501 nayo bei yake ya kikomo imeshuka hadi Sh2840, jambo ambalo linaleta ahueni kwa watumiaji wake.

Kwa upande wa Tanga, petroli kwa bei ya rejareja itaendelea kuuzwa bei isiyozidi Sh3,064 sawa na ilivyokuwa Januari mwaka huu, huku dizeli ikishuka hadi kufikia Sh3,196 kutoka Sh3,219 za Januari.

Watumiaji wa mafuta ya taa mkoani humo nao watapata ahueni baada ya bei ya kikomo kushuka kutoka Sh3,556 hadi Sh2,886.

Kwa wakazi wa Mtwara sasa watanunua lita moja ya petroli kwa bei isiyozidi Sh3,112 kutoka Sh3,201 na dizeli kwa Sh3,196 kutoka Sh3,456 za mwezi uliopita.

Kwa upande wa mafuta ya taa lita bei kikomo nayo imeshuka kwa kiwango kikubwa na sasa watanunua lita moja kwa Sh2,913 kutoka Sh3,582 iliyokuwapo Januari.

Kwa mujibu wa Ewura, kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa kanuni za Ewura za kupanga bei za mafuta za mwaka 2022, zilizotangazwa Januari 28, 2022 kupitia Gazeti la Serikali.

"Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana, yakionesha bei za mafuta, punguzo na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ewura imesisitiza kuwa "ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso