WAZAZI NA WALEZI MKOANI KAGERA WATAKIWA KUWALEA WATOTO ILI HATIMAYE WAKABILI MAZINGIRA NA USHINDANI WA KIMATAIFA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 9 December 2022

WAZAZI NA WALEZI MKOANI KAGERA WATAKIWA KUWALEA WATOTO ILI HATIMAYE WAKABILI MAZINGIRA NA USHINDANI WA KIMATAIFA


WAZAZI na walezi na wadau wote wa mtoto wametakiwa kuwalea watoto wao katika misingi inayofuata malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(MMMAM) kwa miaka 0 hadi nane ili malezi hayo yawawezeshe kuhimili na kukabiliana na mazingira na ushindani kimataifa katika kufanya biashara.



Na Mutayoba Arbogast,Bukoba


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kikao cha Tathmini ya Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM kwa mkoa wa Kagera,ambaye pia ni mganga mkuu wa Mkoa wa Kagera,Dr Issesanda Kaniki,wakati akifungua kikao hicho katika ukumbi wa Ofisi za mkuu wa mkoa,Disemba 09,2022.


Amesema kuwa inafaa kuwalea watoto jwa misingi ya Kitanzania,na hiyo haimaanishi kuwadekeza wala kuwafanya watende kama roboti,bali waandaliwe kuwa raia wema wenye uzalendo kwa nchi yao.


Mtoto wa Kagera,huwezi kumlea kwa kuangalia Kagera tu,bali pia angalia mazingira ya nchi zinazopakana na Kagera na wana maingiliano makubwa na shughuli mbalimbali,ili waweze kuwa tayari kushindana nao katika nyanja za biashara na shughuli mbalimbali.



Wakiwasilisha ripoti za utekelezaji kwa kipindi cha Jula toka Halmashauri za wilaya na manispaa ya Bukoba,maafisa ustawi wa jamii wamesema hakukuwa na bajeti maalum kwa mpango wa PJT-MMMAM 2021/22 kwani wakati mpango huo unaanzishwa,bajeti za halmashauri zilikwishaandaliwa,hivyo bajeti ya 2022/23 MMMAM imehusishwa.


Kuhusu suala la lishe shuleni taarifa zimeonesha kuwa zaidi ya 75% ya wanafunzi wanapata chakula/uji shuleni,huku changamoto ikiwa ni baadhi ya wazazi na walezi kutokuwa tayari kuchangia,licha ya kuwa kunakuwa na ushirikishwaji katika mikutano ya vijiji na Kamati za shule.


Kikao kimeamua kuwa suala la lishe kwa watoto katika mazingira ya nyumbani na shuleni litaendelea kupewa uzito unaostahili,maafisa watembelee maeneo kuliko kutegemea taarifa tu zinazowasilishwa kwao.


Kuhusu ulinzi na usalama wa watoto,washiriki wamesikitishwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia unaotokea katika maeneo yao huku wilaya ya Kyerwa na manispa za Bukoba zikiripoti mtu mmoja mmoja kuhukumiwa kifungo cha maisha kutokana na kesi ya ubakaji.


Afisa ustawi wa jamii wa manispaa ya Bukoba,Shamila Hussein,ameeleza aina mpya ya ubakaji iliyozuka kutokana na tamaa za utajiri,zinazochochewa na waganga wa kienyeji ambapo hata baba mzazi huweza kumnajisi mtoto wake,hata kwa juu juu tu ili mradi 'amemgusa',na hata mtoto anapofikishwa hospitali kwa vipimo,hakuna ushahidi unaoonekana!!


Amesema manispaa imeendelea kupambana na ukatili huo,na kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria.


Salome Frances, kutoka Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia wanawake na makundi maalum, amezihimiza Halmashauri,zinapoandaa mpango kazì,uwe unaotekelezeka na kupimika,kuliko kuweka mambo mengi ambayo hayana uhalisia,na ni vigumu kupimika.


Andrew Nkungu kutoka Tanzania Early Childhood Development Network(TECDEN),mojawapo ya mdau mkubwa katika kuchangia utekelezaji wa PJT-MMMAM,amesema ataliwashilisha ombi la halmashauri za wilaya kuomba kupatiwa mafunzo maalum kufanikisha mpango huo.


Kamati ya uratibu itawasilisha muhtasari wa maazimio kwa mkuu wa mkoa na Wizara ya maenendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum katika kuufanikisha mpango huu unaojumuisha mambo muhimu kwa watoto yakiwa ni elimu,afya,lishe,ujifunzaji wa awali na usalama wa mtoto.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso