MAENEO YA MIPAKANI WATAHADHARISHWA JUU YA UGONJWA WA EBOLA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 26 September 2022

MAENEO YA MIPAKANI WATAHADHARISHWA JUU YA UGONJWA WA EBOLA


Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera,Toba Nguvila(mwenye koti ya lamirabamiraba) akiongea na wananchi kuhusu kujikinga na ugonjwa wa Ebola

TAHADHARI imetolewa kwa wananchi mkoani Kagera wanaoishi maeneo ya mipakani kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa Ebola kwa  kutosalimiana kwa kushikana mikono au kukumbatiana, na  pia kuepukana na mikusanyiko isiyo ya lazima.


Na Mutayoba Arbogast, Huheso Blog - Bukoba


Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila wakati akizungumza na wananchi wa Mwalo wa Kabindi ulioko kijiji Kashenye, kata ya Kashenye wilayani Missenyi.


Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ni kuwa kuna mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Uganda.


“Huku mpakani tunashirikiana vitu vingi, tunashirikiana katika biashara, tunashirikiana shughuli za kiuchumi na tunashirikiana shughuli za kijamii. Kunapotokea maradhi kama haya ya Ebola mazoea yaliyozoeleka ni vema kuchukua tahadhari na kuyazuia kwa muda. Ugonjwa huu sio mzuri ni ugonjwa hatari sana kwasababu kuumwa kwake na muda wa kufa ni mfupi sana hivyo tujali kinga kuliko tiba,” ameeleza Ndg. Nguvila


Sambamba na hayo amewataka Viongozi wa Serikali za Vijiji kuwa mstari mbele na kuhakikisha wanatoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi wao, kudhibiti mwingiliano wa wageni na kueleza kuwa mawasiliano ya haraka yamefanyika na vifaa kwa watoa huduma vimewasili.


Mwenyekiti wa kijiji cha Kashenye,Eustace Makubo alishukuru kwa ujio huo na kuahidi kuzingatia maelezo ya wataalam ili kuhakikisha mwalo huo na wananchi kwa jumla wanabaki salama.


Aidha,akizungumza na mkusanyiko wa wazazi na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Minziro na Watumishi wa kituo cha Forodha cha Mutukula amewasihi kuchukua tahadhari, kuepusha mwingiliano, kuendelea kutoa elimu, kuongeza mabango yanayoelezea elimu juu ugonjwa wa Ebola na kutoa vipeperushi kwa wananchi wanaotumia mipaka hiyo.


Akitoa elimu juu ya dalili za ugonjwa huo Daktari Hassan Kawia ameeleza kuwa ugonjwa wa Ebola unaambukizwa kwa haraka na unaua haraka. Virusi vya ugonjwa huo hukaa kwenye majimaji kama jasho, mate na machozi, unaambukizwa kwa njia kugusana au kukumbatiana. Dalili zake ni homa kali na kutoka damu katika matundu ya mwili kama pua, masikio na macho.


Aidha, amesisitiza wageni wanaoingia kutoka Nchi jirani ni vema wawatolee taarifa ili wafanyiwe uchunguzi na wakionekana na dalili za ugonjwa huo atahifadhiwa sehemu maalum zilizoandaliwa kwa muda wakati akiendelea kupata huduma.


Ndugu Gerasi Ishengoma, Afisa Afya wa Mkoa kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa, amezitaka Zahanati na Vituo vya Afya vya Mpakani kutambua wageni wanaoingia kwenye maeneo yao, kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi.


Kwa mujibu wa Wizara ya Afya,Ebola husababishwa na virusi vya aina ya Ebola na dalili zake  ni homa kali ya ghafla,kulegea kwa mwili,maumivu ya kwenye misuli, kuumwa kichwa,na vidonda vya koo.


Dalili hizi huambatana na kutapika,kuhara, na vipele kwenye ngozi,huku wengine wakitokwa na damu machoni,masikioni,puani,na njia ya haja kubwa na ndogo.


Hivyo inashauriwa kutoshika majimaji au mate au damu ya mtu mwenye ugonjwa,kutoshika mizoga ya wanyama kama popo,sokwe na suala,na iwapo mtu atajihisi kuwa na dalili Anderson mara moja kwenye huduma za afya, na iwapo ataonekana mtu mwenye dalili hizo,taarifa zitolewe kwa serikali za vijiji/mitaa na mamlaka nyinginezo.

Wataalamu wa Afya wakiwa wanatoa maelezo juu ya ugonjwa Ebola kwa Katibu tawala wa Mkoa wa Kagera Ndugu Toba Nguvila

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso