KONGOLE YANGA, SHIKAMOO MPOLE… - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 21 July 2022

KONGOLE YANGA, SHIKAMOO MPOLE…

 


TIMU ya soka ya Yanga imeingia katika orodha ya Klabu   zilizotwaa Ubingwa nchini pasipo kupoteza mchezo hata mmoja. Huku mshambuliaji mzawa George Mpole kutoka Geita Gold FC, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2021/2022.

 

 Na Ali Lityawi


Klabu zingine zilizowahi kutwaa Ubingwa nchini pasipo kupoteza mchezo hata mmoja ni watani zao wa Jadi, Simba Sports Club pamoja na timu ya Azam FC.


Na katika Ligi ya Uingereza maajabu haya yamewahi kufanywa na timu ya Arsenal katika msimu wa 2003/2004 kwa kufikisha alama 90 kwa michezo 38.


Simba Sport Club ikiwa timu ya kwanza nchini kuweka rekodi hii ya kutwaa Ubingwa pasipo kupoteza mchezo hata mmoja katika msimu wa mwaka 2003,ukiwa na kocha Mkenya, Hayati James Siang'a 2009/10, na kurejea rekodi hiyo ikiwa chini ya kocha Raia wa Zambia, Patrick Phiri.


Katika msimu huo ambao Ligi Kuu Tanzania bara ilishirikisha timu 12, Simba ilipata Ubingwa huo toka mikononi mwa watani wao wa jadi, Yanga, walioushikilia ubingwa huo kwa miaka miwili mfululizo.


Simba walipata ubingwa kwa kufikisha alama 62, baada ya kushinda mechi 20 na kutoa sare mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar na African Lyon. Huku mtani wake Yanga akishika nafasi ya pili kwa kufikisha alama 49.


Rekodi hiyo ya Simba ilizimwa na timu ya Azam ikiwa chini ya Kocha raia wa Cameroon, Joseph Omog,kwa kutwaa ubingwa wa msimu wa 2013/14 bila kupoteza mechi na kufikisha alama 62 katika msimu ulioshirikisha timu 14.


Azam katika msimu huo ilishinda mechi 18 na sare nane, huku ikiweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyoifunga timu ya Mbeya City katika uwanja wake wa nyumbani kwa ushindi wa bao 1 – 2.


Baada ya Yanga kuukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo,msimu huu wameubeba toka mikononi mwa watani zao wa jadi Simba walioushikiria kwa misimu minne mfululizo, kwa kufikisha alama .


Yanga wanastahili pongezi kubwa kwa kubeba ubingwa huo pasipo kupoteza hata mchezo mmoja hadi siku walipofikisha pointi zisizoweza kufikiwa na timu nyingine na hadi walipomaliza kabisa ligi.


Katika msimu huu wa 2021/22 ulioshirikisha timu 16,Yanga imecheza mechi 30 na kushinda michezo 22 na kutoa sare michezo minane,ikiwemo miwili ya mtani wake Simba na kufikisha alama 74.


Kwa afya la soka la nchi yetu imekuwa vema Yanga msimu huu kutwaa Ubingwa.Hakuna Ligi bora katika nchi pindi ikitawaliwa na klabu moja,mvuto hupotea.Kwanini timu moja itawale misimu minne mpaka ijisahau?


Ni wazi msimu huu uliomalizika Simba ilianza kwa kusuasua huku Yanga ikiwa ya moto kutokana na usajili mzuri wa wachezaji,benchi la Ufundi na safu ya uongozi. Kwa ujumla muunganiko wa hamasa na ari ya ushindi ilitamalaki kwa klabu hiyo hadi kwa mashabiki wake.


Kwa jinsi hiyo haikuwa shaka kumaliza msimu huku ikiwa na matokeo hayo. Hakika msimu huu ilijipanga hasa, kwani pamoja na dua baya ililoombewa la kupoteza mchezo katika baadhi ya mechi  na mahasimu wao ikawa ndoto.


Ligi kuu ya NBC,msimu huu baada ya Yanga kupata uhakika wa Ubingwa,ilinogeshwa na mchuano wa ufungaji bora,baina ya kinara wa mabao ya Yanga, Fiston Mayele, na mshambuliaji wa timu iliyocheza Ligi kuu kwa msimu wa kwanza; Geita Gold, George Mpole.


Mayele, Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,ameimbwa sana katika mbio hizo za ufungaji bora kutokana na umahiri wake wa kuwatesa walinda mlango wa timu pinzani sambamba na mtindo wa ushangiliaji wake uliokuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki.


Hatimaye pamoja na kuwepo huo mchuano mkali,George Mpole ndiye mshindi wa kiatu cha dhahabu wa Ligi Kuu ya NBC kwa msimu 2021/2022, baada ya kumaliza Ligi kwa jumla ya bao 17, akimuacha mpinzani wake Fiston Mayele mwenye bao 16.


Hongera kwake Mpole, kwa jinsi alivyoudhihirishia umma wa wapenda soka nchini kuwa ni mshambuliaji mahiri hasa kutokana na timu aliyokuwa, lakini amemudu kupambana hadi kufikisha idadi hiyo ya magoli zaidi ya mfungaji bora wa msimu uliopita.


Hata hivyo kinara huyo,haimbwi sana midomoni  kama anavyoimbwa Mayele, kutokana na kutocheza timu kubwa za Yanga ama Simba ambazo zingelisaidia jina lake kuwa sukari midomoni mwa wapenzi wa soka ambao hawaitazami Geita Gold kama timu bora msimu huu.


Mafanikio hayo aliyoyapata Mpole, msimu huu, kusimfanye abweteke bali azidishe mapambano ili kuudhihirishia umma wa soka kuwa hakubahatisha. Anatakiwa ajitambue kazi yake ni soka hivyo asilewe sifa, kwani kwa wapenda soka hawana shaka nae kuwa anajua na anajitahidi.


Wapenda soka nchini wanamtazama kwa jicho la tatu, kwa kufikisha idadi hiyo ya magoli ilhali akicheza timu ndogo. Kwa uwezo aliokuwa nao kama angecheza Simba ama Yanga ambayo imekuwa bora msimu huu, bila shaka angefunga bao zaidi ya hizo.


Baada ya kufika ukomo wa Ligi kuu ya NBC kwa msimu wa 2021/22, timu za Mbeya Kwanza na Biashara ya mkoani Mara zimeshuka daraja huku timu za Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar zikitakiwa kucheza Play Off.


Michezo ya Play Off baina yao  na timu za JKT Tanzania na ….. ndizo zitakazoamua kama zitabaki msimu ujao kucheza Ligi Kuu ya NBC ama kushuka daraja.


Kwa Yanga kukamilika kwa Ligi ya msimu huu kumezidisha rekodi ya kuwa kinara wa soka nchini kwa kutwaa mara 28, lakini je imejipangaje katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika ( CAF Champions League kwa msimu wa 2022/23 ?


Yanga imeiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo kuliko klabu yoyote nchini,lakini hatua ya kujivunia kwa klabu hiyo ni kufikia hatua ya makundi kwa mwaka 1998 na 2016 na mara zote ikimaliza ikiwa ya mwisho, haipendezi.

 

Katika Ligi msimu uliomalizika Yanga Sc, imekuwa bora. Je ubora huo itauendeleza katika michuano ya Kimataifa kama ambavyo watani zao hufanya? Hapa usajili wa maana unahusika. 


Yanga, ina wachezaji tegemezi kama Fei Toto, Mayele, Kibwana, Mwamnyeto, Aucho, Bangala, kati yao wote tegemezi zaidi ni Mayele japokuwa alipokuwa kule Congo, katika michuano hii ya CAF alionekana wa kawaida sana ndio maana ikafikia hatua aje Tanzania.


Hivi Fei Toto, ataweza kuzisumbua timu kama Al Ahly, au Berkane ? Je Mayele tunayemuimba sana atakuwa bora dhidi ya Zesco au TP Mazembe ?  Mwamnyeto na Kibwana Shomari  watendeleza ubora wao dhidi ya Al Masri ama Zamaleki ?.


Kwa kutazama ubora wa timu shiriki katika michuano hiyo toka bara letu la Afrika. Je wachezaji waliokuwa bora katika ligi yetu, watakuwa msaada katika CAF ? Hapana shaka kwa tunaowakubali baadhi watendelea kuwa bora.


Lakini si ajabu katika michuano hiyo ya CAF ikatokea baadhi yao kufichwa na kutokuwa msaada kwa timu hadi kulazimika kutolewa nje ya uwanja,kulingana na ubora wa wachezaji watakaokutana nao katika michuano hiyo.

 

Tusidanganyane ili Yanga kufikia matarajio ya mafanikio katika michuano ya kimataifa lazima kuwe na mipango mkakati, wasijisahau; wajipange vilivyo isije wakawa bora hapa ndani kule CAF ikawa timu mbovu zaidi.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso