BWENI LAUNGUA MOTO WANAFUNZI WAOMBA MSAADA WA MAHITAJI MUHIMU-KAGERA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday 19 July 2022

BWENI LAUNGUA MOTO WANAFUNZI WAOMBA MSAADA WA MAHITAJI MUHIMU-KAGERA

 

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mubaba iliyoko kata ya Kaniha Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, wameiomba serikali na wadau kuwasaidia kupata vitanda, magodoro, mashuka, vifaa vya shule, nguo na mahitaji mengine, baada ya bweni la wasichana kuteketea kwa moto Julai 17 mwaka huu


Jumla ya wanafunzi 135 waliokuwa wakitumia bweni hilo wamepoteza karibia mali zao zote.


Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa moto huo umeteketeza bweni hilo wakati wakiwa wameenda kupata chakula cha usiku, hali iliyosababisha wengi wao kusalia na nguo walizokuwa wamevaa.


“Lakini kiujumla vitu vingi vimeungua na kama mnavyoona wanafunzi hawana hata sare, nyie kama serikali tunaombeni msaada wenu na tunaomba mchukulie hili tatizo kama ni la kwenu mtusaidie ili tupate pa kulala lakini pia kwa kuwa tunakaribia kwenda likizo mtusaidie tujengewe bweni pana na imara zaidi na lenye uzio maana hili lililoungua kulikuwa hakuna uzio” wamesema wanafunzi.


Ili kuhakikisha wanafunzi hao ambao kwa sasa wanalala katika vyumba vya madarasa wanapatiwa msaada wa haraka, mbunge wa jimbo la Biharamulo mhandisi Ezra Chiwelesa kwa kushirikiana na wadau wengine wametoa baada ya vifaa ikiwamo magodoro na mashuka.


“Kwa hatua ya kwanza mimi kama mbunge nimechangia magodoro 50, tunashukuru pia mgodi wa Stamigold wamechangia magodoro 50, kamati ya ulinzi na usalama wamechangia, tumepata madogoro pia kutoka Red Cross kwa hiyo tunaamini upande wa magodoro tutakuwa tumemaliza, na kwa upande wa wadau wa maendeleo wa Biharamulo wa Alsamood wametuchangia mashuka 280, lakini bado uhitaji ni mkubwa kwa sababu watoto hawa wamepoteza kila kitu walichokuwa nacho” amesema Chiwelesa.


Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Kemilembe Lwota amesema kinachofanyika sasa ni kuhakikisha bweni hilo linatengenezwa upya na kuwamba wamepeana siku nne na kazi hiyo itaanza kufanyika kwa kasi ili watoto waweze kurudi katika hali ya kawaida.


“Tunashukuru Mungu tathmini ya awali imefanyika na watoto wetu wanaendelea vizuri na wanaendelea na masomo pia, kwa upande wa usalama bado uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo maana mpaka sasa chanzo halisi hakijafahamika, lakini polisi wanaendelea kufuatilia” amesema Lwota

2 comments:

Post Top Ad

Pages

Huheso