NAMNA YA KUWALINDA WATOTO NA JANGA LA ULAWITI NCHINI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday 29 May 2022

NAMNA YA KUWALINDA WATOTO NA JANGA LA ULAWITI NCHINIUlawiti ni janga linaloendelea kuwakumba watoto nchini, hali ikiwa mbaya zaidi kwa wanafunzi baada ya watoto 30 kutajwa kuhusika kwenye kadhia hiyo hivi karibuni, huku wengine wakilawitiana wao kwa wao, hatua iliyoibua wito wa kitaifa kwa wazazi kuongeza ulinzi na ufuatiliaji wa watoto wao.


Baadhi ya wananchi walizongumza na gazeti hili walisema chanzo cha matendo hayo ni kuporomoka kwa maadili katika jamii, uzembe wa wazazi na ulevi, hasa wa pombe za kienyeji.


Jijini Dar es Salaam juzi kuliripotiwa matukio mawili ya wanafunzi kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono. Mojawapo ni lile la Kinondoni katika Shule ya Msingi Global ambako mwanafunzi mmoja alibainika kufanyiwa mchezo huo na mwalimu wake, ambaye kwa mujibu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, anashikiliwa kwa tuhuma hizo.


Mwalimu wa madrasa, Jumanne Ikungi alifikishwa mikononi mwa vyombo vya dola kwa tuhuma za kuwalawiti wanafunzi wa Shule ya Msingi Mkonoo jijini Arusha hivi karibuni, huku watoto wanane wa Shule ya Msingi Kizota katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakiathiriwa na ulawiti takriban wiki tatu zilizopita.


Katika mkoa huo pia, Diwani wa Mkonoo ilipo shule hiyo, Julius Meori alisema wanafunzi 22 walibainika kufanyiwa ukatili huo na baada ya vipimo, tisa wamebainika kuingiliwa na mmoja kuwa na ugonjwa wa kuambukizwa.


“Tuliwahoji wakasema walikuwa wakifanyia mchezo huo mchafu kwake,” alisema diwani huyo.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema mtuhumiwa bado anashikiliwa kwa mahojiano. “Bado tunamhoji Jumanne, uchunguzi ukikamilika shauri litafikishwa ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka na baadaye mahakamani,” alisema Masejo.


Wakati hayo yakitokea, taarifa za Jeshi la Polisi zinaonyesha ukatili wa watoto kupungua kutoka 15,870 mwaka 2020 hadi 11,499 mwaka 2021, huku asilimia 89 ya ukatili huo ukihusisha vitendo vya ulawiti na ubakaji. Takwimu hizo zimetajwa katika ‘Tanzania Human Rights report 2021’ ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2021.


Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto. Katika mwaka 2020 matukio 7,388 yaliripotiwa kote nchini, tofauti na matukio 5,803 mwaka 2015.


Mkuu wa LHRC mkoani Arusha, Hamis Mayomba alishauri hatua kali kuchukuliwa na uchunguzi ufanyike haraka katika shule za msingi hata sekondari ili wanaobainika kuhusika na unyanyasaji huo wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.


Baadhi ya walimu walitoa rai kwa jamii kuendesha kampeni ya kupiga vita matukio hayo, huku Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda aliyefika shuleni hapo alidai kukamilisha uchunguzi wa tukio lililotokea katika shule hiyo iliyopo pembezoni mwa Jiji la Arusha.


Ulawiti Dodoma

Jijini Dodoma ulawiti uliripotiwa katika Shule ya Msingi Kizota ambako uchunguzi ulibaini watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo hurubuniwa kwa vitu vidogo, huku matukio mengine yakihusisha matumizi ya nguvu kwa watoto hao kupewa vitisho vya kupigwa endapo watatoa taarifa kwa wazazi au walezi wao.


Baadhi ya watoto waliozungumzia tukio hilo wanadai vitendo hivyo hufanyika nyakati za mapumziko shuleni, watuhumiwa wa matukio hayo wakiwataka wakutane chooni.


Joshua Amon (siyo jina lake) alisema wakati anaanza kushiriki vitendo hivyo alikuwa akijisikia maumivu makali, lakini aliogopa kusema kutokana na mazingira ya vitisho huku akiahidiwa zawadi ya biskuti, kujaradia madaftari yao na kalamu za kuandikia.


Mtoto huyo alisema hakuweza kusema nyumbani wala shuleni kwa kutishiwa kupigwa, licha ya kuanza kuhisiwa na mama yake mzazi kabla ya kumshirikisha mfanyakazi wa nyumbani kwao.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kizota, Hamida Mkingule alisema alipokea taarifa ya watoto kwa watoto wa shuleni kwake kujihusisha na vitendo hivyo, hivyo akaiomba Serikali iwajengee uzio.


Mwalimu huyo alisema mwaka jana kulikuwa na matukio matatu, moja likihusisha mwanafunzi wa darasa la pili kuokotwa maeneo ya Mbuyuni akiwa hajitambui baada ya kulawitiwa.


Uchunguzi wa gazeti hili mkoani humo umebaini mbali na shuleni, yapo maeneo hatarishi kwa watoto, ukiwamo Mtaa wa Nzuguni ambako ni maarufu kwa uuzaji wa pombe za kienyeji.


Mwandishi aliyeweka kambi kwenye vilabu hivyo usiku, alibaini watoto wadogo wenye kati ya miaka saba na minane huwaburudisha wateja kuwavutia kununua pombe zinazouzwa na wazazi wao.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Onesmo Lyanga alisema tatizo la kulawitiana kwa watoto limekuwa kubwa katika maeneo mengi, hali inayochangiwa na maendeleo ya utandawazi duniani hata nchini.


Kamanda Lyanga alisema polisi kwa kushirikiana na wananchi, walimu na viongozi wa dini wataendelea kutoa elimu na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo.


Ofisa Mtendaji Kata ya Kizota, Martha Lyimo alisema watoto wanaotokea maeneo ya Relini huiga tabia za baadhi ya ndugu zao walioathirika na mihadarati hata kuwa vibaka, wezi, mashoga au kujihusisha na uuzaji mwili.


Martha alisema kwa kushirikiana na Polisi Kata, wamedhamiria kufanya msako wa wahalifu na vijana wasio na kazi maalumu ili iwe mfano kwa watoto wa maeneo hayo kuacha tabia zisizo na maadili.


Mwenyekiti wa Kata ya Nzunguni B’, Jackson Chidawali alisema changamoto za watoto kulawitiana katika Shule ya Msingi Nzuguni B’ imedhihirika na wanaishughulikia.


Chidawali alisema Machi mwaka huu, Serikali ya mtaa kwa kushirikiana na polisi waliwakamata watoto wanane shuleni hapo na kuwapeleka kituo cha polisi walikokiri kujihusisha na mchezo huo mbaya kwao.


Mkasa wa Iringa

Tukio la ulawiti pia liliripotiwa Machi mkoani Iringa, ambako Jeshi la Polisi linamshikilia mtoto wa miaka 14 kwa tuhuma za kuwalawiti watoto wenzake 19. Mtoto huyo anadaiwa kuwarubuni wenzake kwa pipi na biskuti kukamilishe mpango wake wa kuwalawiti.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alisema mtoto huyo alikamatwa baada ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kihesa Kilolo, Elizabeth Lugenge kutoa taarifa za watoto watatu wa Shule ya Msingi Igeleke kulawitiwa. Alisema baada ya mahojiano, watoto hao walikubali na kuwataja wenzao watano.


Wanasaikolojia

Mwanasaikolojia Charles Mhando alisema moja ya mambo yanayowasababisha watoto kuingia katika vitendo vya kulawitiana ni kukua kwa utandawazi, pamoja na mazuri mengi wanayojifunza wanahitaji kusimamiwa, vinginevyo wanapata nafasi ya kujifunza matendo maovu.


“Kupitia utandawazi watoto wanajifunza mengi mabaya na mazuri, inawezekana ameonyeshwa au ameona video za matendo maovu au amesikia watu wakizungumza na anaweza kushawishika kufanya, hasa wanapokuwa katika kipindi cha kubalehe,” alisema.


Alisema ni muhimu wazazi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, hasa kwa watoto wanaobalehe, kwani mara nyingi hupenda kujaribu mambo mengi.


Mwanasaikolojia mwingine, Josephine Tesha alisema watoto wanaopitia ukatili huo huathirika kiakili, huku wakiwa hatarini kupata ugonjwa wa sonona unaosababishwa na msongo wa mawazo kiasi cha kufikia hatua ya baadhi yao kutaka kujitoa uhai kwa kushindwa kupata majibu ya maswali wanayojiuliza.


Alitaja madhara mengine kuwa ni mtoto kupata homa za mara kwa mara, ikiwamo kuumwa kichwa, tumbo na maumivu ya mwili kwa muda mwingi.


Wanaharakati

Akizungumzia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili, Ofisa Jinsia wa LHCR, Getrude Dyabene alisema vitendo vya ukatili, hasa kwa watoto mara nyingi hufanyika hata ndani ya familia.


“Hii inatokana na ukweli kwamba watoto huwa wanamuamini mtu wanayemjua kwa kufikiri hawezi kuwadhuru ndio maana mara nyingi matukio haya hufanyika ngazi ya familia,” alisema Getrude.


Ongezeko la matukio hayo alisema linatokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya masuala ya ukatili, japokuwa mwamko wa kutoa ripoti juu ya matukio hayo unazidi kuongezeka siku hadi siku.


“Bado hakuna elimu ya kutosha juu ya sheria zinazomlinda mtoto, baadhi ya jamii bado haziheshimu usawa wa kijinsia,” alisema.


Jambo jingine linaloongeza matukio hayo alisema ni matatizo ya akili ambayo baadhi ya watu katika jamii hawajayapa kipaumbele. Alisema ili kuyadhibiti ni vyema elimu ya sheria iendelee kutolewa katika jamii.


Mbali na elimu, Getrude amesisitiza kuimarishwa kwa mfumo wa utoaji haki na ulinzi kwa watu wanaotoa taarifa juu ya matukio ya ukatili pindi yanapojitokeza.


“Hii inasababisha baadhi ya familia za waathirika wa matukio hayo kuamua kuyamaliza masuala hayo nyumbani, jambo linalorudisha nyuma mapambano dhidi ya matendo hayo,” alisema.


Ofisa Ustawi wa Jamii na Mratibu wa Kituo cha Mkono kwa Mkono katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, Asia Mkini alishauri kufanyika kwa utafiti utakaowezesha kujua sababu halisi za kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, hasa yale ya kingono. “Wakati umefika Serikali na jamii kwa ujumla kufanya utafiti kujua sababu za kuongezeka matendo ya ukatili, ni muhimu kuwekeza katika utafiti,” alisema Asia.


Viongozi wa dini

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema kanisa hilo lina sera ya kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili na wanaitekeleza kupitia wataalamu na kufanya kazi kwa ukaribu kuhakikisha mtoto anapata haki zake zote muhimu.


“Kwa anayebainika kukengeuka basi anachukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vinavyohusika kwa hatua za kisheria, hata kwenye baraza tuna dawati maalumu na yupo padri anayesimamia masuala hayo,” alisema Padri Kitima.


Mpasuko kwenye ndoa nyingi na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi pamoja na changamoto za mila na desturi alisema vimesababisha ombwe kubwa la kutokuwaunganisha wanandoa na watoto muda wote, jambo linawaacha watoto wengi kuangukia kwenye ukatili ambao ungeepukika kama mzazi angekuwa makini kuwafuatilia watoto.


“Zamani hata baba akienda kutafuta kazi kulikuwa na babu, bibi au shangazi waliokuwa wanasaidia malezi ya watoto na uangalizi ulikuwa wa karibu, lakini sasa hivi lazima tukubali mifumo yetu ya elimu ya awali na msingi imechukua jukumu la wazazi kuhakikisha malezi yanasimamiwa kwa weledi,” alisema padri huyo.


Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim alisema mmomonyoko wa maadili kwa ujumla umeongezeka, ikiwamo watoto kulawitiwa na mbaya zaidi matendo hayo yanafanywa hata na watu wanaojiita viongozi wa dini.


“Kwa maana ya walimu wa madrasa na Sunday schools nao wamo kwenye tuhuma hizi, jambo hili linaumiza mno. Ninachokiona hapa, pamoja na kuharibu taswira ya viongozi wa dini, wanapaswa kutazamwa wao wala si kwa dini zao, kwani hakuna dini inayoelekeza kufanya uchafu wa aina hiyo,” alisema Sheikh Salim.


Matendo hayo alisisitiza kuwa ni ya kishetani na kwamba kwa viongozi wote wanaotuhumiwa, kuna haja ya kuanza kuwaangalia kama kweli ni walimu au ni mapandikizi wanaojiingiza katika maeneo ambayo hayawahusu.


“Matendo haya nimeyashuhudia na si mara ya kwanza kwa walimu wanaoitwa wa madrasa, kuna wengine wamechukuliwa hatua hata kufungwa gerezani,” alisema.


Alisisitiza haja ya kuanzisha uchunguzi kwa masheikh wa mikoa kuwaangalia walimu wanaofundisha madrasa kama ni wataalamu kweli kwasababu wanaweza kuwa na walimu wanane lakini mwalimu wa kweli ni mmoja tu, hao wengine wamejichomeka.


Mratibu wa Huduma za Makundi Maalumu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Daniel Sendoro alisema hakuna habari mpya, kwani matendo hayo yalikuwapo, tofauti iliyopo kwa sasa inatokana na ukuaji wa teknolojia ya habari iliyofungua fursa ya kuyataja na kuyazungumza kwa upana katika jamii.


Alisema matendo hayo ni ukengeufu wa maadili unaotokana na madhara ya afya ya akili, huku akibainisha wengi wanaotekeleza vitendo hivyo si ushirikina, bali wana matatizo ya akili.


“Lakini kuna harakati zinazofanywa na taasisi za kikahaba duniani mabazo zinajaribu kupandikiza kwa watoto waone mambo hayo ni kawaida, hivyo shule zetu haziko salama na baadhi ya walimu si salama, wamepandikizwa,” alisema mchungaji huyo.


Kauli ya Serikali

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema kulingana na matukio yanayoendelea kujitokeza ya vitendo vya kikatili kwa watoto amebaini wazazi wengi hawakai na watoto wao.


“Mtoto anarudi kutoka shule anafika nyumbani anajikuta yuko peke yake, wazazi wote wapo kwenye mihangaiko ya uchumi hivyo wanakosa muda wa kumkagua mtoto na kuongea naye,” alisema Dk Gwajima.


Waziri Gwajima pia alisema amebaini kamati za ulinzi wa wanawake na watoto kwenye maeneo husika haziko imara, kwani zinatakiwa kushirikiana na wazazi katika malezi ya watoto.


“Wakishirikiana wataweza kubaini watoto wanaoishi mazingira hatarishi, wakiwamo waliomo katika mazingira ambayo kwa wakati mwingine wazazi wao hawapo nyumbani lakini hata elimu ya uelewa kwenye jamii bado ni mdogo,” alisema.


Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa 1989 zinaelekeza ulinzi kwa mtoto, huku Sheria maalumu kuhusu unyanyasaji wa kingono (SOSPA) ya mwaka 1998 inaelekeza adhabu kwa makosa ya kujamiiana, ikiwamo kutoa tafsiri ya matukio ya ulawiti na ubakaji.


Imeandikwa na Mariam Mbwana, Tuzo Mapunda na Nasra Abdallah (Dar), Musa Juma (Arusha) na Shakila Nyerere (Dodoma).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso