SHIRIKISHO la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) limetengua agizo la kuzivunja Bodi za Vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS) 335 mkoani Simiyu ambalo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila kwa vile halikuzingatia taratibu za ushirika.
Mwenyekiti wa TFC Taifa, Gishuli Charles amesema agizo hilo ni batili na ametangaza rasmi viongozi wote wa Bodi waendelee kutekeleza majukumu yao kama kawaida.
Tamko la Mwenyekiti Gishuli limetolewa baada ya kuwasikiliza viongozi mbalimbali wa AMCOS kwenye kikao cha dharura ambacho kimefanyika makao makuu ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Simiyu ambapo anaeleza.
Kwa upande wao wawakilishi wa Muungano wa Vyama vikuu vya ushirika vinavyojishughulisha na zao la Pamba nchini (TANCCOOP), Kwiyolecha Nkilijiwa na Deogratias Didi wametoa wito kwa viongozi wa AMCOS kusimamia kikamilifu shughuli za ushirika.
Baadhi ya viongozi wa Bodi za AMCOS wakiwemo, Cosmas Luchagula na Masuke Nindi kutoka Chama cha Msingi cha Ushirika OMAU Old Maswa mkoani Simiyu wamesema hawana taarifa zozote kuhusiana na agizo la Mkuu wa mkoa wa Simiyu na kwamba hakuna mkulima ye yote anayevidai vyama vyao kama inavyodaiwa na mkuu huyo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Simiyu, Kulwa Samwel amesema ofisi yao haijapoke barua na haina taarifa zozote za kuvunjwa kwa Bodi za Amcos mkoani Simiyu,.
Mei 5,2022 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mheshimiwa David Kafulila alichukua uamuzi mgumu wa kuwatimua kazi maofisa ushirika wa halmashauri sita.
Halmashauri hizo ni Bariadi Mjini, Bariadi Vijijini, Maswa, Busega,Itilima,Meatu zote za Mkoa wa Simiyu.
Sambamba na kuvunja uongozi wa AMCOS 335 alisisitiza kuwa,bei ya pamba mkoani Simiyu inakwenda kuvunja rekodi ya miaka 30 huku akieleza kuwa, zao la pamba Mkoa wa Simiyu linapaswa kuheshimiwa na watu wote.
"Kwanza inafahamika Simiyu ndio Simba wa Pamba Tanzania ikizalisha wastani wa asilimia 40 hadi 60. Pamoja na bei nzuri msimu uliopita kufikia shilingi 1800, bado kuna malalamiko mengi yaliyothibitika mchezo mchafu kati ya AMCOS na Maofisa Ushirika uliosababisha mkulima kutopata bei halisi iliyolipwa na mnunuzi.
"Aidha uchunguzi wa PCCB (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kuhakiki kila AMCOS kuona vielelezo kuthibitisha malipo aliyolipwa mkulima na kiasi ambacho AMCOS iliuza pamba kwa niaba ya mkulima.
"Mpaka sasa zimechunguzwa AMCOS 189 na zote hakuna vielelezo kuthibitisha malipo sahihi kwa mkulima,"ameeleza Mheshimiwa Kafulila.
No comments:
Post a Comment