TANZANIA YAZIDI KUNG'ARA KIMATAIFA: DIPLOMASIA YA SAMIA YALETA MATOKEO CHANYA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 27 May 2026

TANZANIA YAZIDI KUNG'ARA KIMATAIFA: DIPLOMASIA YA SAMIA YALETA MATOKEO CHANYA


Taswira na heshima ya Tanzania katika nyanja za kimataifa imeendelea kuimarika kwa kasi kubwa kutokana na utekelezaji wenye tija wa sera madhubuti za mambo ya nje na diplomasia ya uchumi.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alibainisha hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.


Alieleza kuwa katika utekelezaji wa vipaumbele vya wizara na kwa kuzingatia malengo ya kimkakati, serikali imepata mafanikio makubwa yaliyotokana na kuimarika kwa ushirikiano wa uwili uliowezesha upatikanaji wa rasilimali fedha, ujuzi, na teknolojia kutoka mataifa rafiki pamoja na fursa mbalimbali kupitia mikataba na hati za makubaliano zilizosainiwa.


Waziri Kombo alifafanua kuwa ushirikiano wa kikanda umeendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa itifaki na programu za mtangamano zenye maslahi makubwa ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii kwa taifa la Tanzania.


Katika uwanja wa ushirikiano wa kimataifa, nchi imeendelea kushiriki kikamilifu katika ajenda zote kuu zinazohitaji juhudi za pamoja duniani ikiwemo utunzaji wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, kusukuma mbele ajenda ya nishati safi ya kupikia, mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko, na kuzuia uhalifu unaovuka mipaka, hatua inayothibitisha utayari na mchango wa nchi katika maendeleo ya kimataifa.


Kutokana na ushawishi huo mkubwa, Tanzania imefanikiwa kupata nafasi mbalimbali za kimkakati katika jumuiya za kikanda na kimataifa, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, huku Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiteuliwa kuwa Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, sambamba na Balozi Stephen Mbundi aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Mbali na hayo, mchango wa Watanzania waishio nje ya nchi yaani Diaspora umeendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa katika kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo fedha, uwekezaji, nyumba, kilimo, na viwanda.


Balozi Kombo alihitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali imeendelea kuwa imara katika kulinda usalama wa raia wake wote waliopo nje ya nchi, ikifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuratibu na kutekeleza urejeshwaji wao salama nyumbani kutoka maeneo yote yaliyokumbwa na vita au machafuko ya kisiasa duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso