WAZIRI WA MADINI, MHESHIMIWA ANTHONY MAVUNDE, amesema Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) iko mbioni kuanza ujenzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya dhahabu katika eneo la wachimbaji wadogo la Mwakitolyo wilayani Shinyanga, mkoani Shinyanga, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo Jumatatu, Desemba 22, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye mgodi wa Mwakitolyo Namba Tano, Waziri Mavunde amesema mtambo huo utakuwa na uwezo wa kuchenjua tani 100 hadi 120 za madini ya dhahabu kwa siku na unatarajiwa kuwahudumia zaidi ya wachimbaji wadogo 7,900 wa Mwakitolyo pamoja na migodi ya jirani.
Amesema ujenzi wa mtambo huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika pamoja na teknolojia rafiki ya uchenjuaji wa madini.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa maelekezo mahsusi kwa Wizara ya Madini kupitia STAMICO kuhakikisha wachimbaji wadogo wanasimamiwa na kuwezeshwa hivyo tayari eneo la ujenzi limepatikana katika Kijiji cha Mawemelu, na ujenzi utaanza hivi karibuni,” amesema Mavunde.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 serikali imepanga kujenga mitambo mitatu ya uchenjuaji wa madini, ikiwemo miwili ya dhahabu itakayojengwa Mwakitolyo mkoani Shinyanga na Buhemba, pamoja na mtambo mmoja wa chumvi.
Amesema lengo la miradi hiyo ni kuongeza thamani ya madini yanayochimbwa na wachimbaji wadogo, kupunguza upotevu wa madini na kuongeza mapato kwa wachimbaji na Taifa kwa ujumla.
Awali, akitoa kero kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Albert Bahame amemuomba Waziri wa Madini kuingilia kati suala la umiliki wa maeneo wanayochimba, akieleza kuwa wachimbaji wamekuwa wakifanya shughuli za uchimbaji kwa zaidi ya miaka 30 bila kuwa na uhakika wa umiliki wa kisheria.
“Tangu mwaka 1995, kumegunduliwa na kuanza uchimbaji wa dhahabu katika eneo la mlima wa Namba Sita, shughuli hizi zimefanywa na wachimbaji wadogo ambao tumekuwa tukilipa kodi zote za serikali, hata hivyo, kumekuwepo na taarifa kuwa eneo hilo linamilikiwa na mwekezaji ambaye hatujawahi kumuona,Tunaomba tupewe leseni za uchimbaji mdogo ili tufanye kazi zetu kihalali,” amesema Bahame.
Naye Charles Boniface, mchimbaji katika mgodi wa Namba Sita Mwakitolyo, amesema ucheleweshwaji wa utoaji wa leseni umekuwa kikwazo kikubwa kwa wachimbaji wadogo, kwani unawafanya kukosa uhakika wa shughuli zao na kushindwa kuchangia kikamilifu pato la Taifa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Sheria ya Madini Sura ya 123, Waziri Mavunde amesema Kifungu cha 8 kinaweka zuio kwa raia wa kigeni kuingia katika leseni za uchimbaji mdogo, akisisitiza kuwa sheria hiyo inalenga kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo Watanzania.
Amesema, “Kifungu cha 8(3) kinaeleza kuwa iwapo kutahitajika msaada wa kiufundi, basi unatakiwa kutolewa kwa taratibu maalum bila kuhatarisha umiliki wa leseni za wachimbaji wadogo. Hili tunalisimamia kikamilifu.”
Aidha, Waziri Mavunde ameielekeza Tume ya Madini kufuta leseni zote ambazo hazijaendelezwa kwa mujibu wa sheria, akieleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakihodhi maeneo ya madini bila kuyaendeleza, hali inayozuia fursa kwa wachimbaji wenye nia na uwezo wa kufanya shughuli za uchimbaji.
Amesema maeneo yatakayofutiwa leseni yataandaliwa upya na kugawiwa kwa vikundi vya vijana na wanawake kwa ajili ya uchimbaji mdogo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) inayolenga kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini.
Mwisho.










No comments:
Post a Comment