SERIKALI YATOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 300 KUBORESHA MIUNDOMBINU SHULE YA MSINGI TUNDURU MCHANGANYIKO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday 5 May 2024

SERIKALI YATOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 300 KUBORESHA MIUNDOMBINU SHULE YA MSINGI TUNDURU MCHANGANYIKO









Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru Sabina Lipukila akiongea na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba wa shule hiyo juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya elimu inayojengwa katika shule hiyo baada ya serikali kutoa zaidi ya Sh.milioni 300.
Nyumba ya kuishi familia mbili za walimu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko iliyojengwa kwa fedha kutoka serikali kuu ambayo itawawezesha walimu kuishi karibu na eneo lao la kazi.


Na Mwandishi wetu
Tunduru

SERIKALI imetoa kiasi cha Sh.milioni 302 ili kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi na walimu katika shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sabina Lupukila amesema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 246 zimetoka serikali kuu na Sh.milioni 56 zimetolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru.
- Advertisement -


Lipukila alisema,Sh.milioni 80 zimetumika kujenga bweni,Sh.milioni 50 kujenga nyumba moja ya walimu ya familia mbili,Sh.milioni 60 kujenga uzio na Sh.milioni 56 kwa ajili ya matundu 32 ya vyoo.

Aidha alieleza kuwa,Sh.milioni 56 zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru, Sh.milioni 41 zimetumika kumaliza ujenzi wa miradi hiyo iliyoanzishwa na serikali kuu na Sh.milioni 15 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Alisema,bweni lina uwezo wa kuchukua watoto 80 na katika awamu ya kwanza litatumika kulala watoto wa kike wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kujenga bweni lingine la watoto wa kiume.

Alisema, kwa sasa shule ya Tunduru Mchanganyiko ina wanafunzi 1,738 kati yao wanafunzi 43 ni wa elimu maalum kuanzia darasa la awali hadi la saba ambao wanatoka nyumbani na kwenda shule kila siku.

Lipukila alisema,ujenzi wa bweni hilo ni mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuwajali watoto wenye mahitaji maalum na kuboresha mazingira ya elimu ili kuhamasisha watoto kupenda kusoma na wazazi kupeleka watoto wao shule kwa ajili kupata haki yao ya msingi.

Alisema,serikali inatambua umuhimu wa kuwa na mazingira mazuri ya kusoma ili kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalum kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.

Alisema, bweni hilo ni dawa itakayotibu watoto wote wenye mahitaji maalum waliopo katika wilaya ya Tunduru kutopenda kusoma na wengine kuacha shule kwani sasa kuna sehemu nzuri na rafiki itakayowawezesha kutimiza ndoto zao.
“watoto wenye ulemavu sio kwamba hawana ndoto,lakini changamoto kubwa imetokana na mazingira magumu kwa baadhi ya wazazi,natoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto wenye mahitaji maalum wawalete watoto wao kwenye shule hii”alisema.

Mratibu elimu kata ya Mlingoti Mashariki Erith Banda,ameishukuru serikali kujenga bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum na nyumba moja ya kuishi walimu.

Alisema,bweni hilo litamaliza adha kwa watoto wanaoishi mbali na shule kutumia muda mrefu kila siku kwenda kufuata masomo na kuepukana na changamoto mbalimbali za njiani

Ambilikile Mwandembo anayefundisha watoto wenye ulamavu alisema,watoto hao wamegawanyika kwenye makundi matatu ambayo ni walemavu wa akili,ulemavu wa kusikia,mabubu,wenye uono hafifu na walemavu wa ngozi.

Alisema,watoto walemavu wanafundishika hivyo wazazi wachae tabia na kasumba ya kuwaficha watoto hao nyumbani,badala yake wawapeleke shule wakapate haki yao ya msingi.

Samia Shabani mwanafunzi wa darasa la saba alisema,bweni hilo ni muhimu sana kwa wenzao wenye ulemavu kwani sasa watapata muda mwingi wa kusoma kwa sababu wataishi shuleni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso