MWANAFUNZI ALAWITIWA WILAYANI NGARA AKIENDA SHULE, AMTAMBUA MHUSIKA MARA TATU KWENYE GWARIDE LA UTAMBUZI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday 29 May 2023

MWANAFUNZI ALAWITIWA WILAYANI NGARA AKIENDA SHULE, AMTAMBUA MHUSIKA MARA TATU KWENYE GWARIDE LA UTAMBUZI



Jeshi la polisi wilayani Ngara, mkoani Kagera, linamshikilia kijana aitwaye Niyombele Ndayisenga mkazi wa Kijiji cha Nyabisindu kata ya Kabanga wilayani humo kwa tuhuma za kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka sita, mwanafunzi wa darasa la kwanza (jina lake na shule anayosoma vinahifadhiwa), wakati akielekea shuleni.


Na Mutayoba Arbogast, HUHESO DIGITAL BLOG, Bukoba


Kwa mujibu wa Afisa habari wa SMAUJATA (Shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania) wanaoendesha Kampeni ya kupinga ukatili chini ya Wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum), wilaya ya Ngara Juvenary Ilambona, ametoa wito kwa wadau wote wanaohusika na watoto kuendelea kuwalinda, na kufichua vitendo vya ukatili dhidi yao.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mkoani Kagera, amesema tukio hilo lilitokea Mei 9 mwaka huu, ambapo kwa ushirikiano wa SMAUJATA na wadau mbalimbali, mtuhumiwa huyo alifikishwa kituo cha polisi Kabanga, ambapo tarehe 26 Mei, 2023,  limefanyika gwaride la utambuzi na mtoto kumtambua mtuhumiwa huyo mara tatu.


Mashujaa hao wa kupinga ukatili, wamemshukuru Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Julius Kahabi ambaye baada ya kumpa taarifa aliwasiliana na vyombo vya usalama kuhakikisha jambo hilo linashughulikiwa kwa haraka.


Ulinzi na usalama wa watoto ni wajibu wa kila mtu kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) ya mwaka 2021/22 hadi 2025/26.


Programu hiyo inahusu watoto wenye umri wa kuanzia miaka sifuri hadi nane katika nyanja za ulinzi na usalama, elimu, afya na malezi yenye mwitikio, katika kuhakikisha watoto wanakua katika hali yenye utilifu.


Ripoti mbalimbali zinaonesha kuendelea kuongezeka kwa vitendo vya ukatili licha ya awali kuwepo Mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWA)  chini ya Ofisi ya Waziri mkuu  uliolenga kupunguza aina zote za ukatili kwa asilimia 50 kufikia mwaka 2022.


Hata hivyo Ripoti ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali(CAJ) ya mwaka 2021/22 baada ya kutembelea mikoa sita, inaonesha kuna ongezeko la vitendo vya ukatili wa kingono, kwa mfano katika mkoa wa Dar es salaam  kufikia mwezi Juni 2022 kulikuwa na matukio 1,656 kulinganisha na matukio 326 yaliyorekodiwa mwaka 2018.


Katika mkoa wa Arusha hadi Juni 2022 kulikuwa na matukio 1,427 kulinganisha na matukio 625 ya mwaka 2018, huku mkoa wa Tabora ukiwa  na matukio 250 kutoka matukio 97 yaliyorekodiwa mwaka 2018.


Taarifa ya  Benki ya dunia ya mwaka 2021 kuhusu Tathimini ya Jinsia nchini Tanzania inaonesha asilimia 30 ya wasichana wanapitia ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18.


Takwimu zilizopo kutoka Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba watoto 537 walilawitiwa nchini kwa mwaka 2016, idadi ambayo imepanda hadi kufikia watoto 1,114 kwa mwaka 2021, ikiwa ni mara mbili ya ile iliyorekodiwa mwaka 2016.


Mradi wa Mtoto kwanza wa Shirika la Children in Crossfire Tanzania, na Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM, wamedhamiria kuboresha, pamoja na mambo mengine, afua za ulinzi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka nane.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso